Breaking News

USHAIRI: "NASUBIRI JIBU LAKO"


Ushairi: NASUBIRI JIBU LAKO.

1. 
Ni tamu sauti yako,
Nifananishe na nini,
Wanivutia mwondoko,
Ka hugusi ardhini,
Natamani huba zako,
Hivi utanipa lini?

2. 
Hilo tabasamu lako,
Mithili ya huraini,
Lanimaliza mwenzako,
Nguvu zaisha mwilini,
Hivi huo moyo wako,
Kunipa washindwa nini?

3. 
Viatu viwe kokoko,
Na hata vya chinichini,
Vyapendeza vyote kwako,
Kila uvaacho hani,
Hivi langu hamaniko,
Tayari shalibaini?

4. 
Nyusi kama zina piko,
Na vishimo mashavuni,
Nuru ya machoni mwako,
Kama nyota za mbinguni,
Hivi langu fadhaiko,
Kiumbe haulioni?

5. 
Mwisho nipa moyo wako,
Milele niuthamini,
Changu kitakuwa chako,
Kweli sifanyi utani,
Nisubiri jibu lako,
Mahabuba hadi lini?

No comments