Breaking News

MAKALA MAALUM: MIAKA 3 YA MAAJABU YA JPM IKULU (Sehemu ya 02)

Inaendelea....

Hata hivyo, mara kadhaa Rais Magufuli licha ya kelele hizo, aliendelea na msimamo wa kuwataka wafanyabiashara kulipa kodi, huku akisisitiza yupo tayari iingie meli moja kila mwezi ambayo italipa ushuru kuliko kuingiza meli mia moja ambazo hazilipi kodi, ambapo mbali na kubaini makontena yaliyopitishwa bandarini bila kulipa kodi, zilibainika meli zaidi ya 60 ambazo ziliingia kinyemela na kushusha mizigo nchini bila taarifa zake kuwekwa kwenye kumbukumbu za bandari na TRA.

Pia kulikuwa na biashara ya makinikia ambapo yalisafirishwa Makontena zaidi ya Elfu Sitini kutokea mwaka 1998 mpaka mwaka 2016 yaliyokuwa yanapelekwa nje ya nchi yetu yakiwa na madini ya aina mbalimbali kama dhahabu na kopa kwenda nje ya nchi Suala lingine ambalo amelishughulikia kwa kipindi kifupi cha utawala wake wa Awamu ya Tano, na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma na kutumia fedha alizookoa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ambayo ilikwama kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa fedha ambazo zilikuwa zinaliwa na baadhi viongozi wa Serikali ambao hawakuwa waadilifu wa mali za umma. 

Matumizi mengine ambayo amefanikiwa kuyadhibiti ni safari za nje ambazo hazikuwa na tija zilizokuwa zinafanywa na watumishi wa umma, ambapo hivi sasa ili mtumishi asafiri kwenda nje ya nchi, ni lazima apate kibali kutoka Ikulu, huku akiwataka mabalozi kuwakilisha nchi kwenye mikutano na mazungumzo yanayohusu uwekezaji unao husiana na nchi yetu.

Uamuzi wa kuwaachia mabalozi kuiwakilisha Tanzania kwenye nchi ambazo wapo, umelisaidia Taifa kuokoa fedha nyingi maana watumishi walikuwa wanaondoka na kundi kubwa kwenda kuhudhuria mikutano au semina ambazo hazikuwa na tija kwa Taifa letu na ilikuwa kati ya njia zilizokuwa zinapoteza fedha zetu hovyo kazi zile zingeweza kufanywa na mabalozi wetu, lakini hivi sasa tunaona mambo yanavyozidi kubadilika na mabalozi wetu wanatimiza wajibu wao wa kuliwakilisha Taifa, na fedha zinaokolewa na kutumika kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo badala ya kuwanufaisha viongozi wachache waliokuwa wanakwenda nchi za nje kwa ajili ya kujistarehesha.

Hata hivyo kutokana na udhibiti wa makusanyo ya kodi, Serikali imefanikiwa kununua ndege saba zikiwemo kubwa mbili aina ya Boeing 787-8 dreamliner, ndege mbili aina ya Bombadier CS 300 na Bombadier dash8-Q400 tatu na kuanzisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railway) kati ya Dar es Salaam na Morogoro, na kuanza mchakato wa kujenga miondombinu ya mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge Rufiji.

Kwa upande mwingine serikali kwa kutumia mapato yake ya ndani na fedha zilizookolewa kwenye matumizi mbalimblai, imefanikiwa kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari darasa la kumi mbili na kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, huku ikitoa shilingi bilioni 88.764 kwa ajili ya kujenga meli mpya itakayofanya safari kati ya Mwanza na Kagera.

Mbali na kudhibiti safari za nje na kuokoa fedha nyingi, Rais Magufuli amefanikiwa kuwaondoa kazini watumishi hewa ambao walikuwa wanaigharimu Serikali fedha nyingi, sambamba na wanafunzi hewa ambao walikuwa wanapewa mikopo na kuwakosesha nafasi ya kusoma watoto kutoka kwenye familia masikini wenye vigezo vya kupata mikopo hiyo. Katika hatua nyingine, kwenye suala la mikataba,utawala wa awamu ya Tano umefanikiwa kuipitia na kurekebisha mikataba mibovu iliyokuwa inalitia hasara Taifa ikiwemo mikataba ya madini ambayo Kamati zote mbili zilizoundwa kuichunguza zilibaini wizi mkubwa uliokuwa unafanywa na makampuni ya uchimbaji wa madini yaliyopo nchini. 

Katika mapambano dhidi ya rushwa serikali imefanikiwa kudhibiti rushwa kwa kiasi kikubwa na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la kimataifa linaloangalia hali ya Rushwa na mapambano dhidi ya ufisadi duniani(Transparency) imeeleza katika kipindi cha mwaka Mmoja Tanzania imepanda nafasi 13 duniani imesogea kutoka chini kwenda juu ni kutokana na jitihada za Rais Dkt. John Pombe Magufuli na timu yake na Watanzania kwa ujumla.

“Ukifika kwenye ofisi za umma hivi sasa unahudumiwa vizuri bila hata kuombwa rushwa, mfano mzuri ni kwenye mahospitali yetu ikiwemo hospitali kuu ya Muhimbili, kulikuwa na kero kubwa sana na ili upate huduma ulilazimika kutoa rushwa, ukitaka umeme, maji, pasipoti ni lazima utoe rushwa, lakini mambo yamebadilika na huduma zinatolewa bila usumbufu wowote, alisema Magreth Joseph, mkazi wa Ubungo Jijini Dar Salaam.

Magreth alisema wamefarijika kutokanana na kuboreshwa kwa huduma za X-Ray na CT-Scan ambazo awali walikuwa wanalazimika kwenda kuzipata kwenye hospitali za watu binafsi kwa gharama ya juu kwa kile kilichoelezwa, mashine za Muhimbili na kwenye hospitali nyingine za Serikali ni mbovu. 

Katika mojawapo ya nukuu za hayati baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuonya kuwa kiongozi mwadilifu anapochakuliwa kuingia Ikulu ni lazima awaambie jamaa na ndugu zake kuwa “ Ikulu ni mahala patakatifu. Mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza pango la walanguzi na ukishakuwaambia hivyo, ndugu zako na ikajulikana hivyo, mtu mwingine wala hata kusogelea. Nafsi yake haitamtuma kukusogelea” alisema Mwalimu Nyerere kwenye hotuba yake aliyoitoa mwaka 1995.

Hii ni mojawapo ya sababu kubwa ambazo zinamjenga Rais Magufuli kutokana na jinsi anavyoshirikiana na wananchi wake, watendaji wa vyombo vya dola na watumishi kwenye maeneo mbalimbali ndio maana anapata taarifa nyingi za mambo yanayoendelea kila siku nchini na kuchukua hatua za haraka sambamba na kurudisha heshima ya Ikulu. 

Rais. Magufuli ametuonyesha watanzania uzalendo wake baada ya mama Janeth Magufuli alipougua alilazwa Kwenye Hospitali ya Muhimbili katika wodi ya Mwaisela na akiwa (First Lady) kitendo ambacho watanzania hatujawahi kushuhudia Ma “First Lady” kulazwa katika hospitali zetu hapa nchini lakini hata hivyo hivi juzijuzi dada yake mkubwa Monika alilazwa katika hospitali ya Bugando na kupotezea maisha yake katika hospitali hiyo kitendo ambacho viongozi Wengine hawakuwahi kufanya hivyo, walikuwa wanawapeleka nje ya nchi.

Watanzania wenye mapenzi mema tumuunge mkono kwa dhati Rais wetu kwa namna anavyowaenzi waasisi wa Taifa letu kuanzia Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Sheikh Abeid Amani Karume aliyekuwa Rais wa Kwanza na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na viongozi mashuhuri wa Kitaifa kama aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Edward Moringe Sokoine, hivi karibuni mheshimiwa Rais alifanya ziara kanda ya ziwa alipotembelea mkoani Mara katika wilaya ya Butiama alitoa ahadi ya vitendo kuikarabati shule ya Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa na kulihakikishia Taifa kuwa atafanya ukarabati wa barabara inayopitia Butiama na kufanya marekebisho mbalimbali katika mji aliozaliwa Baba wa Taifa.

Pamoja na mambo mengine Rais Duwe na majengo mazuri, ukarabati wa miundo mbinu kama maji, umeme na barabara kwa kiwango cha lami. Pia aliahidi kukarabati uwanja wa ndege wa Musoma uwe katika kiwango cha lami ili ndege za aina nyingi ziweze kutua.

Amejenga fly over ya Tazara iliyobatizwa kwa jina la Mhandisi Patrick Mfugalle ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Tanroads Tanzania nzima, alipewa heshima hiyo kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu mbalimbali hapa nchini.

Hivi sasa tunashuhudia ujenzi wa fly over nyingine katika eneo la ubungo ambayo ujenzi wake unaenda haraka. Madhumuni ya fly over hizi ni kupunguza msongamano wa magari katika njia kuu ya Dar es Salaam – Morogoro, Mandela na Sam Nujoma. 

Pia tunaendelea kushuhudia upanuzi wa barabara kutoka Kimara kuelekea Kibaha Mailimoja, barabara hiyo itakuwa na njia nane (8) ambayo itarahisisha kupunguza foleni katika eneo la njia kuu muhimu kwa uchumi wetu kwani mataifa mengi kama Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi, Congo DRC, Zimbabwe mataifa hayo ni watumiaji wakubwa wa barabara ya Morogoro.

Wahisani kutoka mataifa mbalimbali ya nchi za Ulaya magharibi na mashariki, Marekani, Asia, Mashariki ya kati na Jamhuri ya watu wa China wanaridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano kwa uadilifu wa mali za umma ikiwemo misaada wanayoitoa inatumika kwa njia zinazostahili.

Pia amekiimarisha Chama cha Mapinduzi, viongozi kuwa na nidhamu ya utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2015. Watanzania pia wanazidi kukiamini chama cha mapinduzi na wengi wao hivi sasa wanazidi kumiminika kurudi chama cha mapinduzi wakiwemo waheshimiwa wabunge na madiwani.

Makala imeandaliwa na:
Japhet Mwandimo
Afisa Mstaafu JWTZ

No comments