AFYA: SABABU 6 ZA KWANINI MARA NYINGI WANAWAKE HUISHI ZAIDI YA WANAUME
Mara nyingi tumeshuhudia katika familia nyingi mwanaume akitangulia kufa kabla ya mwanamke. Simaanishi kuwa wanaume wote wanakufa mapema, lakini mara nyingi wanawake huishi zaidi kuliko wanaume.
Swala hili limepelekea kuibua shauku ya kufanya utafiti zaidi juu ya sababu za wanaume wengi kufa mapema kuliko wanawake.
Kwa kuwa lengo la Fahamuhili.com ni kukupa maarifa, basi karibu ufahamu kwanini mara nyingi wanawake huishi miaka mingi zaidi ya wanaume.
1. Wanawake hujali afya zao zaidi
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa afya zilibaini kuwa wanawake hujali afya zao zaidi. Tafiti hizo zinaeleza kuwa wanawake wengi wanapojihisi kuumwa huenda hosipitalini ili kupata ushauri wa kitaalamu.
Hali ni tofauti kwa wanaume, kwani wao huvumilia maumizu au hata kutumia dawa bila kupata vipimo na ushauri wa kitaalamu. Hili limepelekea kufupisha maisha ya wanaume wengi kwani huwa hawatambui maradhi hatari mapema.
2. Wanaume huendeleza tabia hatarishi zaidi
Tabia kama vile uvutaji wa sigara, pombe au madawa ya kulevya mara nyingi hufanywa na wanaume. Hili limepelekea kuathiri afya zao kwa kiasi kikubwa na kusababisha kufupisha maisha ya wanaume wengi.
3. Wanaume hujiua zaidi kuliko wanawake
Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa kiwango cha vifo vinavyotokana na kujiua kwa wanaume ni kikubwa kuliko kwa wanawake.
Kutokana na changamoto mbalimbali wanaume wengi huchukua maamuzi ya kujiua. Lakini wanawake wengi huvumilia changamoto hizo badala ya kujiua.
4. Wanawake wanapenda kushirikisha watu wengine
Kuna usemi usemao “mwanaume ana kifua cha kutunza mambo”; kwa hakika kwa upande mwingine hili ndilo huchangia wanaume kufa mapema.
Wanawake wanapokuwa na tatizo huwaeleza watu wengine ili wawashauri au hata wawasaidie. Lakini mwanaume atavumilia tatizo kwa kujipa moyo kuwa huo ndio uanaume.
Swala hili humwathiri mwanaume ndani kwa ndani na hatimaye kusababisha matatizo kama vile shambulio la moyo au kiharusi.
5. Maradhi ya moyo huchelewa kutokea kwa wanawake
Tafiti zilizofanywa huko Marekani, zilibaini kuwa maradhi ya moyo huua wanaume na wanawake lakini maradhi haya huchelewa kwa takriban miaka 10 kwa mwanamke.
Hivyo wanaume wengi wanapata maradhi ya moyo mapema zaidi kuliko wanawake.
6. Kazi wanazofanya wanaume zinawachakaza
Naamini swala la kazi ngumu au hatari kwa wanaume linafahamika wazi, wanaume hufanya shughuli za shuruba bila hata kupumzika au kula vyema.
Kazi hizi huwachakaza wanaume na kuwafanya wafe mapema ikilinganishwa na wanawake ambao wengi hawafanyi kazi ngumu sana za shuruba.
Neno la Mwisho
Kwa hakika uhai wa mtu uko mikononi mwa Mungu, lakini kuna badhii ya mambo huchangia kufupisha uhai wa mtu. Ikiwa wewe ni mwanaume na unaweza kuyaepuka badhii ya mambo yaliyoelezwa hapa, basi fanya hivyo ili angalau uongeze siku kadhaa.
No comments