Breaking News

UINGEREZA YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA, BENKI YA DUNIA YATOA USHAURI NAMNA YA KUWEKEZA KWENYE VIWANDA

Waziri Kakunda akiwa na Balozi wa Uingereza, Sarah Cooke

Timu ya wataalam elekezi wa Benki ya Dunia (WB) wameishauri Tanzania kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata mazao ili kuongeza thamani ya kilimo kwa lengo kumkomboa Mtanzania.

Watalaam hao jana Jumatatu Januari 28, 2019 wamekutana na waziri wa viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na kumueleza kuwa ipo haja ya kuongeza nguvu katika eneo hilo ambalo kwa sasa linaonekana bado halikufanyiwa kazi vya kutosha.

Waziri Kakunda amekiri udhaifu huo na kueleza kuwa kumekuwa na changamoto lukuki zinazokwamisha uchakataji wa mazao nchini kubwa ikiwa ni ukosefu wa malighafi jambo linalosababisha viwanda vya aina hiyo visiwepo.

Alisema kwa sasa uchakataji wa mazao umekuwa wa kusuasua kutokana na upatikanaji wa mazao hivyo Serikali inafungua milango kwa wawekezaji kuja kuwekeza kwenye viwanda vya aina hii ili kuchakata mazao hapa na bidhaa kuuzwa nje.

“Wametushauri vitu vingi kubwa likiwa ni kutuhamasisha kuweka nguvu kwenye uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao. Inatakiwa tuwe tunauza nje ya nchi bidhaa ambayo imeshatengenezwa si malighafi,” alisema.

“Tukiboresha mazingira ya biashara tupata wawekezaji wengi na kuongeza mapato kwa Serikali kwa sababu watu wengi watahitaji kufanya biashara Tanzania,” alisema.

Katika hatua nyingine Waziri Kakunda amekutana na Balozi wa Uingereza, Sarah Cooke ambaye alimueleza kuwa nchi yake imedhamiria kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka Uingereza kuja Tanzania.

Balozi huyo ameeleza Uingereza itaongeza nguvu katika elimu ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalam wengi watakaofanya kazi kwenye viwanda.

Kwa upande wake, Waziri Kakunda amemueleza Cooke kuwa Serikali itaviwezesha viwanda vinavyomilikiwa na Waingereza ili viendelee kufanya kazi na kutoa ajira kwa Watanzania na kuzalisha bidhaa zitakazobeba nembo ya Tanzania.

No comments