MAAFISA MAENDELEO YA JAMII MIKOANI WAJIPANGA KUPAMBANA NA UKEKETAJI
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi.Grace Mwangwa akizungumza na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara wakati akifungua kikao kazi kilichowakutanisha Maafisa Maendeleo ya Jamii hao kujadiliana na kupata mpango mkakati wa kutokomeza ukeketaji kilichofanyika mjini Morogoro.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi Bw. Emmanuel Burton akielezea kuhusu Mpango Mkakati wa kutokomeza ukeketaji kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara utakaohusisha Maafisa Maendeleo ya Jamii hao kupambana na vitendo vya ukeketaji katika maeneo yao kilichofanyika mjini Morogoro.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara Bi. Neema Ibamba akichangia katika kikao kilichowakutanisha Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Mikao 26 ya Tanzania Bara kujadiliana Mpango Mkakati wa kutokomeza ukeketaji kilichofanyika mjini Morogoro.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Dodoma Bi Honoratha Rwegasira akichangia katika kikao kilichowakutanisha Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara kujadiliana Mpango Mkakati wa kutokomeza ukeketaji kilichofanyika mjini Morogoro.
Maafisa Maendeleo ya Jamii kutpka Mkoa 26 ya Tanzania Bara wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika kikao kilichowakutanisha Maafisa hao kujadiliana Mpango Mkakati wa kutokomeza ukeketaji kilichofanyika mjini Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Grace Mwangwa akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Mkioa 26 ya Tanzania Bara na Maafisa Kutoka Wizarani mara baada ya kikao kilichowakutanisha Maafisa Maendeleoya Jamii hao kujadiliana Mpango Mkakati wa kutokomeza ukeketaji kilichofanyika mjini Morogoro.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu Morogoro
Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Sektretarieti za mikoa wamejipanga kupambana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto hasa vitendo vya ukeketaji katika mikoa yao ili kuondokana na vitendo hivyo.
Hayo yamebainika katika kikao kazi kilichofanyika mjini Morogoro leo kilichowakutanisha maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara kwa lengo la kujadiliana na kuweka Mikakati ya kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto hasa vitendo vya ukeketaji.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Grace Mwangwa amesema kuwa Wizara imewakutanisha Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara kwa lengo la kuandaa Mkakati wa kutokomeza ukeketaji kwa ajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ambao utatekelezwa na Maafisa Maendeleoya Jamii hao katika mikoa na Halmashauri za Mikoa yao.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa Mkakati huo wa kupambana na ukeketaji utaenda sambambamba utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto bali ndio utakuwa msaada wa kutekeleza mpango huo ili kuwezesha kuondokana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Dodoma Bi.Honoratha Rwegasira amesema kuwa kwa Mkoa wa Dodoma una vitendo vingi ya Ukeketaji na kama Mkoa wamejipanga kuondokana na vitendo hivyo na Mpango huo ukikamilika utamsaidia kuongeza mbinu zaidi za kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Ameongeza kuwa mpaka sasa wamewajengea uwezo watendaji katika Wilaya za Chamwino, Kongwa na Mpwapwa katika kuweza kutekeleza Mpango Mkakati wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hasa vitendo vya Ukatili.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara Bi. Neema Ibamba amesema kuwa Mkoa wa Mara umejiapanga katika kutokomeza vitendo vya ukatili hasa katika wilaya za Tarime na Serengeti na Serikali ya Mkoa na Wilaya hizo zimejidhatiti katika kutoa elimu na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaobainika kufanya vitendo hivyo.
Pia Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita Bw. last Lingson amesema kuwa Serikali na wadau wanapaswa pia kuangalia mikoa ambayo ina asilimia ndogo katika vitendo vya ukeketaji na vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwani kuna uhamaji wa watu kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine hivyo kuhama na mila na desturi zao zikiwemo mila za ukeketaji na kufanya kuongezeka kwa vitendo hivyo katika maeneno ambayo hayakuwa na vitendo hivyo.
No comments