Breaking News

MAKALA YA LEO: NINAMUONA THOMAS SANKARA NDANI YA RAIS JOHN MAGUFULI

Na Francis Daudi 
+91 9513833624(Whatsapp tu)
__________________________________________
Historia ya Afrika imejaa visa vingi vya simanzi, Hata baada ya miaka 50 ya Uhuru bado nchi za Afrika zimeendelea kutegemea misaada ya nje! Cha ajabu hata wanapotokea viongozi wachache wazalendo wamekuwa wakikumbana na kila aina ya uadui. Mara nyingi huchafuliwa na hata kuondolewa madarakani kwa nguvu kubwa ya ‘mabeberu’ wakishirikiana na baadhi ya ‘Vibaraka’. Mmoja kati ya Viongozi waliopata kupinduliwa Afrika huku ikieleweka wazi ni njama mbaya za vibaraka ni Thomas Sankara.

Thomas Sankara alikuwa kiongozi na raisi akiwa na miaka 33 lakini mwenye maono makubwa na siasa za mrengo wa kushoto, anatambulika sana kama "Che of Africa"-‘Che wa Afrika’ akifananishwa na Ernesto Guevara ambaye alikuwa mwanamapinduzi huko Amerika Kusini. Thomas Isidore Noel Sankara alizaliwa Desemba 21 mwaka 1949 nchini Burkina Faso, iliyotambulika Kama Upper Volta kwa wakati huo. 

Wakati wa mafunzo ya kijeshi alikutana na kapteni Blaise CompaorƩ, wakawa marafiki wakubwa. Hivyo mwaka 1983, waliongoza mapinduzi yaliyoiondoa serikali ya kidhalimu madarakani na kuiweka serikali mpya yenye mitizamo ya kijamaa. Sankara alikuwa raisi mpya lakini Octoba 15 mwaka 1987 alipinduliwa na Blaise CompaorƩ akishirikiana na mabepari ambao waliiona Burkina Faso ikibadilika kimaendeleo.
__
Thomas Sankara

Ni wazi kuwa ndiye rais pekee Afrika Magharibi ambaye anakumbukwa zaidi. Thomas Sankara, akiwa Kama raisi ndani ya miaka minne tu aliibadilisha Burkina Faso kutoka kuwa nchi masikini na inayotegemea misaada mpaka kuwa taifa imara linalojitegemea kiuchumi na kijamii. Na hapo ndipo nnaona maono yake kwa raisi wa Jamhuri ya Muungano Mweshimiwa John Joseph Magufuli. Ndani ya miaka mitatu amefanya maamuzi mazito ya kiutawala, kiuchumi na hata kijamii kuhakikisha Tanzania inatoka kuwa nchi tegemezi kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Kama ilivyo kwenye miaka mitatu ya Mweshimiwa Magufuli, Thomas Sankara alianza kwa kupambana ili kuing’oa mizizi ya urasimu na rushwa iliyokuwa imekithiri huko Burkina Faso. Serikali ya Magufuli ina ufanano mkubwa na ile ya Sankara hasa katika kubana Matumizi, Sankara alipunguza mishahara ya mawaziri na kuuza magari yote ya kifahari yaliyotumiwa ikulu, kisha akanunua gari la bei ndogo tu, Renault 5. Mshahara wake ulikuwa dola 450 sawa na shilingi 958,005 za kitanzania.

Sankara alikuwa raisi wa wanyonge na watu masikini kama Magufuli. Hakutaka maisha ya anasa na starehe kama marais wengine! Wakati Fulani, Sankara alikataa kutumia viyoyozi (air conditioning) kwani alijiona kama mwenye hatia, hii ni kwa sababu ni watu wengi katika nchi yake walikuwa hawezi kununua wala kuvitumia. Huyu ndiye Sankara ninayemuona ndani ya rais wa Tanzania. 

Maendeleo aliyoyaleta Thomas Sankara kwa nchi ya Burkinafaso hayaelezeki kwa maelezo mafupi. Mwaka mmoja tu wa utawala wake, Sankara aliongoza utolewaji wa chanjo kwa watoto milioni mbili na nusu wa nchi hiyo. Vifo vya watoto wanaozaliwa vilikuwa ni vya kutisha. Kati ya watoto 1000 waliozaliwa, zaidi ya 280 walifariki chini ya umri wa miaka mitano na kufikia vifo 145 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa ndani ya mwaka mmoja.

Sankara alisisitiza nchi ‘kujitegemea’, alipiga marufuku uingizwaji wa bidhaa toka nje ambazo zingeweza kutengenezwa Burkina Faso. Hii ilisaidia ukuaji wa viwanda vidogovidogo, haikuchukua muda wabukinabe walianza kuvaa nguo zilizotokana na pamba iliyolimwa ndani ya nchi yao. Pia alizuia uingizaji wa mchele na nafaka zingine toka Ulaya. Haya yanafanyika chini ya utawala wa rais Magufuli, Katibu wa wizara ya kilimo ndugu Mathew Mtigumwe juzi alieleza wazi kuwa serikali ya Tanzania imesitisha kabisa uingizaji wa Mchele hapa Tanzania kwani mahitaji ni tani 900,000 na mchele uliopo ni tani milioni 2.2. Tanzania imekuwa nchi ya tano kusini mwa jangwa la Sahara kwa uzalishaji wa mchele mwaka huu 2018 baada ya Nigeria, Madagascar, Mali na Guinea.

Sankara alibadili jina la nchi lililoachwa na wakoloni la Upper Volta na kuiita Burkina Faso yaani nchi ya ‘waburkinabe’ ikimaanisha ‘Ardhi ya watu wenye misimamo’. ‘Makabaila’ waliojimilikisha ardhi kubwa walipokonywa na ikagawanywa upya kwa wakulima wadogowadogo. Rais Magufuli pia amekuwa akiguswa na migogoro ya ardhi na kadhia wanazokumbana nazo wananchi wa kawaida. Wakati wa ziara yake Mkoani Mara alimpigia simu Mh. Lukuvi(Waziri anayeshughulikia ardhi). Hii inaonyesha kwa namna gani anavyojali wananchi wanaoonewa.

Ndani ya miaka mitatu, Sera ya Elimu bure inayotekelezwa na Serikali ya Magufuli imepata mafanikio makubwa. Kila mwezi serikali inayoongozwa na Rais Magufuli imekuwa ikitenga bilioni 18 kwa ajili hiyo. Huyu ni Sankara nnayemuona ndani ya Magufuli kwani pia miaka miwili aliyoingia madarakani Sankara, maudhurio ya wanafunzi mashuleni yalipanda toka asilimia 10 mpaka asilimia 90. Sankara alitaka elimu iwe bure kabisa hili linafanywa kwa vitendo na serikali iliyochini ya Magufuli.

Miezi 12 ya utawala wake, Sankara aliongoza upandwaji wa miti milioni 10 ili kupunguza madhara yaliyotokana na kuongezka kwa Jangwa la Sahara. Sankara alisisitiza wanawake kupewa hadhi wanayostahili hata katika jamii zilizokuwa na mfumo’DUME’ ambapo wanawake wengi waliajiriwa hata kwenye zile nafasi nyeti. Ili kujenga mshikamano alitangaza siku maalumu ambayo wanaume walipaswa kuwasaidia kazi zote za nyumbani wake zao.

Hakuwa raisi ‘legelege’, Kama ilivyo kwa Magufuli, Sankara alikuwa mtu wa ‘kazi tu’. Sankara alitaka wananchi wake kufanya kazi kuliko kulalama tu. Haikushangaza alipoonekana mara kwa mara asubuhi katika mitaa ya jiji la Ouagadougou akifanya mazoezi hata kushiriki usafi na shughuli zingine za maendeleo.

Mwaka 1987, wakati wa kikao cha viongozi wa umoja wa nchi za Afrika, Sankara alijaribu kuwashauri viongozi wenzake kukataa mikopo ya kifedha toka mataifa ya magharibi. Alisisitiza kuwa mikopo na misaada ya kifedha inarudisha ukoloni barani Afrika.

‘…..mikopo inatufanya kila mmoja wetu kuwa mtumwa wa fedha za magharibi’, sera na masharti ya mikopo na fedha za misaada inatufanya tutengane, inatudhalilisha na kutupora uwezo wetu wa kuwajibika ili kujiimarisha kiuchumi, kisiasa na hata kiutamaduni. Inahatarisha juhudi zetu katika kujitegemea ili kupata maendeleo endelevu. Hatuwezi kuendelea kwa misaada ya kifedha!

Inaelezwa kuwa alikuwa mtu wa maamuzi ambayo ni magumu, lakini pia mara nyingi alifokea hata mawaziri na wafanyakazi wazembe. Hakupenda rushwa na aina zote za unyonyaji. Baada ya mapinduzi ya 1987, Blaise CompaorƩ alifuta sera zote za utaifishaji na kukubali masharti yaliyowekwa na mashirika ya kimataifa ya fedha. Kwa namna hii ndio maana Blaise CompaorƩ anaelezwa kama kibaraka aliyetumwa kumuondoa rafiki yake wa siku nyingi ili tu kufungua njia za unyonywaji wa rasilimali za nchi ya Burkina Faso. Mpaka sasa Blaise CompaorƩ anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Thomas Sankara mara baada ya kuondolewa madarakani.

Maono ya Thomas Sankara yalikuwa ni Waafrika wawe pamoja ili kujiletea maendeleo yao. Alipinga bila uoga udhalimu waliofanyiwa watu wa Afrika ya kusini ambao kwa kipindi hicho walikuwa chini ya serikali ya makaburu waliotekeleza sera ya ubaguzi wa rangi. Alimuambia wazi raisi wa Ufaransa wa kipindi hicho Jacques Chirac kuwa anakosea kuiunga mkono serikali ya kikaburu pindi raisi huyo alipotembelea Burkina Faso. 

Alikuwa mjamaa na mwafrika mwenye uchungu na hali ya wananchi wake, mpaka anauawa kwa kupinduliwa alimiliki gari, Jokofu, magitaa matatu na akiba ya dola 400 tu. Namuona Sankara kupitia Magufuli. Nayaona maono yake kupinga ufisadi na kutetea raslimali zetu za Afrika kupitia Magufuli. Amehakikisha mikataba yote inapitiwa upya ili kuhakikisha nchi inanufaika. Alizuia makontena ya makinikia mpaka utaratibu unaoweza kufaidisha pande mbili ulivyowekwa. Magufuli amekuwa akikemea wazi wazi wabadhirifu na kufukuza kabisa watendaji wanaotetea maslahi yao! Sankara alianzisha mahakama ya wananchi iliyoitwa ‘People’s revolutionary tribunals’ kushughulikia watendaji wala rushwa na wabadhirifu wa mali za umma. Hakuna tofauti kubwa na Mahakama ya Mafisadi ambayo inalenga kutoa hukumu kwa wote wanaokutwa na hatia za ufisadi.

Wakati wa ziara yake mikoa ya kanda ya ziwa, Nimeweza kumwona vizuri Sankara ndani ya rais wetu John Magufuli. Sankara akielezea falsafa yake katika kuleta mabadiliko ya wananchi alipata kusema ‘You can not carry out fundamental change without a certain amount of Madness’ akimaanisha ‘Huwezi kuleta mageuzi ya kimsingi kama hauna kiwango Fulani cha ukichaa’. Sankara alisema hayo mwaka 1985, Huko Ukerewe, Rais Magufuli aliweka bayana kuwa alimteua Waziri Mpina kwani ana ‘Ukichaa’ ndani yake. Akiwa na maana kuwa ni waziri ambaye anaweza kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Ni kama vile Sankara anazungumza ndani ya Magufuli.

Wiki moja kabla ya kupinduliwa, katika kumbukumbu ya Che Guevara, Sankara alisema ‘Wanamapinduzi wanaweza kuuawa lakini mawazo yao mazuri hayatakufa kamwe’. Ni kama vile alijua siku moja mawazo na maono yake yatapata mtu wa kuyalinda na kuyatetea. Leo anakumbukwa kama mtu mwenye uadilifu mkubwa, mkweli na mwenye msimamo wa kueleweka tofauti na viongozi wengi wa Afrika wa sasa.

Ni wazi kwamba, mabepari na ‘vijibwa’ wao wanatumia nguvu kubwa kuhakikisha Sankara na mawazo yake yanafutika Afrika. Magufuli ameonesha dhahiri ndani ya miaka mitatu jinsi anauishi ‘Usankara’ kwa vitendo. Uwekezaji kwenye miradi mikubwa kama ununuzi wa ndege, treni za kasi, umeme na kwenye elimu unathibitisha nia yake ya dhati nchi kwenda kwenye uchumi wa kati na wa kiviwanda. Hii itasaidia kupunguza utegemezi kwa nchi wahisani na hivyo kuwa na taifa lenye kujitegemea na kuheshimika Zaidi ulimwenguni.

Imeandaliwa na:
Francis Daudi
Mwanahistoria na Mdau wa Maendeleo
0768035253

No comments