MAKALA MAALUM: MIAKA 3 YA MAAJABU YA JPM IKULU (Sehemu ya 01)
"YAFUTA MAKOSA YA WATANGULIZI WAKE"
Na Japhet Mwandimo
Tangia Rais Dk.John Magufuli aingie madarakani Novemba 05, 2015 imerejesha Heshima ya Nchi yetu Kitaifa na Kimataifa kutokana na uchapakazi wake katika kuwatumikia watanzania wa kada zote sambamba na kulinda rasilimali za Taifa pamoja na kurudisha maadili kwa watumishi wa Umma.
Ni ukweli usiopingika kwamba kila mtanzania mwenye akili timamu na mapenzi mema kwa nchi yake atakuwa amejionea kasi ya ajabu iliyoonyeshwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Dk.John Magufuli.
Hii ni kutokana na ukweli usiopingika kwamba amefuta makosa yaliyofanyika katika awamu zilizopita kwa kuvaa viatu na fikra za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alipenda kuiona Tanzania inapiga hatua katika kila Nyanja kwa kupambana na Rushwa pamoja na kurejesha maadili kwa watumishi wa umma ambayo yalikuwa yamepotea kwa kiasi kikubwa.
Kutokana na hali hiyo Rais Dk. Magufuli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuondoa miradi hewa ambayo ni uzao wa ufisadi ambao umezalishwa na ufisadi ulioasisiwa na viongozi wa ngazi za juu ya nchi yetu wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara watanzania wenzetu wenyewe pamoja na wale wenye asili ya kiasia pamoja na wanyonyaji wengine walioingia kwa kupitia mlango wa nyuma katika kuhujumu juhudi za serikali yetu kwa kipindi kirefu.
Aidha viongozi wetu wa ngazi za juu walikuwa wakiamrishwa wafanye kama wanavyotaka wafanyabiashara wakubwa ambapo hiki ndio chanzo cha matatizo yetu ya kushamiri miradi hewa, ufisadi na rushwa kutokana na udhaifu wa baadhi ya viongozi wa Serikali katika Serikali za awamu ya pili mpaka Serikali ya Awamu ya nne.
Hapa ndipo watendaji wa daraja la kati la Serkali na wao walipopata mwanya wa kufanya madhambi kwani walijua kilichokua kinaendelea ndani ya Serikali na hasa kutokana na viongozi wa ngazi za juu kujihusisha moja kwa moja na ukosefu wa maadili ya uongozi.
Baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu Serikalini walividhoofisha vyombo vyetu vya Usalama ambapo TAKUKURU waliondolewa meno ya kuwauma wahalifu waliokuwa wakishirikiana nao katika miradi hewa na UFISADI wa mali za Umma.
Baadhi ya nchi za kiafrika ambazo rushwa na ufisadi vilishamiri na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu walikuwa vinara wa kuiba mali za umma nchi hizo za Kiafrika kama GHANA, AFRIKA YA KUSINI, ZAIRE, KENYA, ANGOLA na kwingine na wananchi wa nchi hizo walianza kutoa malalamiko mbalimbali dhidi ya baadhi ya watawala wa nchi hizo na baadhi ya viongozi wa nchi hizo walipoteza maisha au kuondolewa madarakani kwa nguvu.
Taifa lifanye nini ili kuweza kumsaidia Rais Dk. John Magufuli ili kuimarisha mapambano ya kutokomeza UFISADI, RUSHWA, MIRADI HEWA, UADILIFU NA UZALENDO.
Pamoja na kwamba vyombo vyetu vya Usalama vinajitahidi sana kupambana na wahalifu mbalimbali wa mali za umma kiundwe chombo kitakachomsaidia Mhe. Rais ili kutoa taathmini halisi ya mapambano ya vita hiyo ambayo ni ngumu kuitokomeza kwa haraka kwa kuwa viongozi wengi na wafanyakazi wa Serikali katika ngazi mbalimbali waliishiriki katika madhambi hayo ya wizi wa mali za Umma.
Mapendekezo ya wazee walioonyesha Uadilifu wa Uongozi ambao hawakuyumba waliendeleza uadilifu wao katika awamu zote kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza hadi Serikali ya awamu ya tano, wapo wazee ambao hawana kashfa yeyote katika utumishi wao wa umma kama mzee Joseph Butiku Mzee Job Lusinde, mzee Salim Ahmed Salim,Jaji Joseph Sinde Warioba na Jaji Augustino Ramadhani wengine wengi ambapo ni hazina kwa taifa letu.
Watanzania tukumbuke muda mfupi baada ya kuapishwa na kuingia Ikulu ya jijini Dar es Salaam Novemba 5, mwaka 2015 Rais Magufuli alianza kushughulikia suala la ukwepaji kodi ambao kwa siku za nyuma ulikuwa umekithiri na kuikosesha Serikali mapato.
Moja ya maendeleo ambayo alianza kuyashughulikia kwa siku za awali akiwa Ikulu, ni Wizara ya Fedha ambayo ndio inasimamia mapato ya nchi nzima kupitia kodi na makusanyo mbalimbali. Baadhi ya wananchi waliongea na waandishi wetu kwa nyakati tofauti wakimsifu kiongozi huyo kwa kazi nzuri anayoifanya tangu ashike nafasi ya kuongoza nchi yetu.
Nakumbuka Rais Magufuli aliwahi kusema kwamba,anajua mambo yanayoendelea Wizara ya Fedha hususani Hazina, alisema wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano bajeti zilikuwa zinapitishwa bungeni kiholela, lakini fedha zilikuwa hazitoki kwa wakati.
Nadhani hilo lilikuwa linafanyika kwa sababu kuna baadhi ya watumishi wasio waaminifu walikuwa wanaingiza fedha hizo kwenye mizunguko yao ya kibenki au katika biashara zingine ili wapate faida na kuchelewesha miradi muhimu ya maendeleo alisema Jafari Salumu, mkazi wa Temeke Dar es Salaam.
Rais Magufuli alimuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim afuatilie utendaji wa kazi kwenye maeneo muhimu ya bandari ya Dar es Salaam, ambalo ni lango kuu kwa uchumi wa nchi yetu na kubaini makontena 2431 ambayo yalipitishwa kinyemela kupitia bandari kavu bila kulipiwa kodi.
Kufuatia ziara hiyo ya Waziri Mkuu, Rais Magufuli alitangaza kumuondoa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rished Bade na Mkurugenzi Mtendaji wa Bandari (TPA) Awadhi Massawe na baadae akatangaza safu mpya iliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti matumizi mabaya ya bandari hiyo na kuongezeka kwa mapato.
“Wakati anaingia madarakani Rais Magufuli alikuta mambo ya hovyo yanaendelea bandarini, ilifikia hatua hadi wafanyabiashara wa nchi za jirani kama Rwanda, Zambia, Malawi, Congo DRC, Burundi na Uganda walikuwa wanaiogopa bandari yetu ya Dar es Salaam kwa sababu mizigo yao ilikuwa inaibiwa mno katika magari na makontena yaliyokuwa yanapotea na baadhi ya vifaa vilikuwa vinaibiwa ndani ya magari yao”alisema mmoja wa wafanya biashara Godfrey Charles mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Kuna baadhi ya wafanya biashara walikuwa wanauza bidhaa zao kwa bei ya chini sana, kwa sababu walikuwa hawalipi kodi inayostahili, walikuwa wanatuumiza sana wafanya biashara tuliokuwa tunalipa kodi inayostahili, biashara ilikuwa ngumu mno ila kwa hivi sasa wafanya biashara wote tunalipa kodi ile ile na bei za bidhaa zipo sawa sokoni, ingawa wao na na baadhi ya vibaraka wao walikuwa wanapiga kelele kwamba, makontena bandarini yamepungua sana, kwa sababu ya kutozwa kodi kubwa na Serikali ya awamu ya tano“ aliongeza kwa kusema mkazi huyo wa Kinondoni.
Itaendelea tolea lijalo....
Makala imeandaliwa na
Japhet Mwandimo
Afisa Mstaafu - JWTZ
No comments