Breaking News

MAKALA MAALUM: “KUIMARIKA KWA MISINGI YA UCHUMI WA TANZANIA NA MIAKA 3 YA MAGUFULI”


Na Debora Charles 

Ni dhahiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza malengo yake makuu 5 iliyojikita nayo ambayo yanachochea mwelekeo wenye tija katika kuifikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Mfano tumeshuhudia suala la uimarishaji wa miundombinu ya kimkakakati (Strategic infrastructure) kama vile SG railway, Stiglier’s Gorge na Flyovers -DSM.

Serikali imeendelea kukuza uchumi na kupunguza umasikini, kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, kujenga nidhamu ya utendaji kazi pamoja na kuimarisha mahusiano ya kimataifa.

Kwa kufuatilia Hotuba ya Mhe. Rais Magufuli na hotuba ya Prof. Kabudi katika kongamano la “Kutathmini kwa kina juu ya hali ya Uchumi na Siasa Tanzania” lililofanyika tarehe 01, Novemba 2018 katika Chuo kikuu cha Dar Es Salaam pamoja na Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Serikali 05, Novemba 2018, nimebaini mambo yafuatayo;

Kumekuwa na Ongezeko la ukuaji wa Uchumi. Mwaka wa fedha wa 2017/2018 uchumi wetu umekuwa kwa kiwango cha asilimia 7.1, ukuaji huu umepelekea Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi 9 duniani ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Dunia pamoja na World Economic Forum. 

Katika kipindi hiki, zaidi ya viwanda 3,066 viliandikishwa; vinaendelea kujengwa na baadhi vimekamilika na vinatoa bidhaa mbalimbalimbali pamoja na ajira. Kati ya hivyo 251 ni vikubwa na vya kati ni 173. Tayari mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2015 hadi 5.5 mwaka 2017.

Nchi yetu imeendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kwa ajili ya mahitaji yake. Mpaka sasa akiba yetu ni wastani wa $ Bil 5.4, haijawahi kutokea tangu nchi ipate uhuru. Fedha hii inaweza kuendesha nchi kwa kununua bidhaa kwa kipindi cha karibu miezi 6. 

Makusanyo ya kodi ya serikali yameongezeka kutoka wastani wa TShs Bil 850 kwa mwezi kwa mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa TShs Tril 1.3 kwa mwezi kwa mwaka 2018. 

Kipindi cha nyuma malipo ya fedha ya mshahara kwa watumishi wote kwa mwezi yalikuwa ni TShs Bil 777. Baada ya kutolewa watumishi hewa waliokuwa ni zaidi ya watu 34,000 mishahara ilirudi kuwa TShs Bil 251 kwa mwezi. Hatua hizi zimesaidia taasisi zilizokuwa zinashare na serikali kulipa kutoka Tshs Bil 249 hadi Bil 717.2 mpaka sasa. 

Kumekuwa na Ongezeko la fedha kwenye Bajeti Serikali ya Maendeleo kutoka chini ya asilimia 20 hadi asilimia 40 kila mwaka. Ongezeko hili limepelekea kuwepo kwa miradi mingi inayotekelezwa. 

Ujenzi wa Reli mpya ya kisasa (Standard Gauge). Mpaka sasa zimetumika pesa za kodi za wananchi TShs Tri. 7.06 kutoka Dar Es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Dodoma. Kadharika serikali imeweka mpango wa kuunganisha Reli ya Standard Gauge katika nchi za Rwanda (Isaka hadi Kigali) na Burundi (Kuanzia Tabora hadi Kigoma) kwa lengo la kuzifanya nchi zinazotuzunguka zitumie bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni mkakati wa kuimarisha uchumi.

Upanuzi wa Bandari za Dar es Salaam pamoja na Tanga ambapo pia linajengwa bomba refu la mafuta lenye urefu wa KM 1400 kutoka Ohima-Uganda hadi Tanga-Tanzania. Kadharika upanuzi wa bandari ya Mtwara unaolenga kurahisisha uingizaji wa bidhaa kama mafuta kutoka Dar Es Salaam hadi Mtwara.

Ununuzi wa meli kwenye ziwa Victoria. Serikali inategemea kununua meli yenye thamani ya zaidi ya TShs Bil 89 katika ziwa Victoria. Kadharika ukarabati wa meli zingine kama Mv Victoria, Mv Butiama, Mv Lyemba na meli zingine katika ziwa Victoria. 

Serikali inategemea kuwa na ndege zetu wenyewe 7 ambapo mpaka sasa 4 zimekwisha ingia nchini na zingine 2 aina ya Airbus zinatarajiwa kufika hivi karibuni, na Dreamliner nyingine 1 mwakani ikiwa lengo ni kukuza sekta ya utalii na uchumi.

Kuongezeka kwa wanafunzi wanojiandikisha kujiunga na masomo ya msingi kutoka wastani wa milioni 1.5 hadi kufikia milioni 2. Ongezeko hili limetokana na serikali kutekeleza sera ya elimu bure ambapo mpaka sasa kiasi cha fedha kinachotolewa na serikali ni TShs Bil 23.85 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure. Kadhalika Mikopo ya wanafunzi Vyuo vikuu mikopo imeongezeka kutoka bil 367.4 hadi bil 483. 

Mapato katika sekta ya madini yameongezeka, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini, serikali ilitegemea kukusanya TShs Bil. 194 kwa mwaka, badala yake serikali ilikusanya TSh Bil 301 kwa mwaka wa fedha 2017/18 (hii ni mara 2 zaidi ya kiwango kilichotarajiwa). Mabadiliko haya ya Sheria ya madini yalifanyika mwaka 2016 ambapo yalifuatiwa na kanuni zake 2017.

Mpaka sasa serikali imenunua Radar ambazo zitafungwa katika maeneo yote ya Tanzania. Jambo hili litaongeza pato la Taifa kwa sababu ndege zote zitakazokuwa zinapita katika anga letu zitalipia, kadhalika ulinzi na usalama kwa nchi utaimarika kwa sababu tutakuwa na uwezo wa kusimamia anga yetu wenyewe. Vile vile anga ya nchi yetu itaaminika kwa mataifa mengine hivyo watapitisha ndege zao kutokana na sababu za kiusalama na hii itaimarisha sekta hii (Aviation Industry).

Utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme unaotokana na nguvu ya maji katika mto Rufiji (Stigler’s Gauge) ambao mpango wake uliasisiwa na Mwl Nyerere. Umeme huu ndiyo umeme wa bei rahisi kuliko mwingine wowote. Gharama za Umeme huu ni TShs 36 per unit pekee, jambo hili ni tofauti ukilinganisha na vyanzo vingine ambapo gharama za umeme wa jua na upepo TShs 114.2 per unit, gesi ni TShs 118 per unit, Themo kutoka ardhini ni TShs 114.2 hadi 216 per unit na mafuta ni TShs 547 per unit. 

Kadhalika umeme huu utakaotumia vyanzo vya maji utazalisha umeme mwingi ambao utakuwa ni kwa wastani wa zaidi ya MegaWatt 2100. Mpaka sasa jumla ya Megawatt 1560 tu za umeme ndizo zinazozalishwa japo kuna hatua zinaendelea za kuongeza Kinyerezi I na II. Hii itasaidia kukidhi mahitaji ya wananchi kutokana na ongezeko la watu na viwanda, ambapo mpaka sasa kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi 2012 Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya mil 55 ukilinganisha na watu mil 10 kipindi cha uhuru.

Kuongezeka kwa Bajeti ya Kuboresha huduma za afya kutoka TShs Bil 31 kwa mwaka 2015/16 hadi Bil 269 kwa mwaka 2017/18. Ujenzi na ukarabati wa hospitali za wilaya (vituo 295). Ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya 306, ongezeko la upatikanaji wa dawa muhimu pamoja na kunzishwa kwa tiba za kibingwa kwenye hospitali za serikali.

Vile vile ongezeko la usimamizi wa mali za Taifa, uimarishwaji wa ulinzi na usalama, mapambanao dhidi ya rushwa, Kuhamishia Makao Makuu Dodoma, Kurudisha nidhamu katika utendaji wa kazi na kupambana na matumizi ya ubadhilifu vimeimarishwa.

Ni ukweli usiopingikia kuwa hali ya Maendeleo ya sasa katika sekta ya viwanda, kwa kiasi kikubwa imejibu hoja nyingi zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya sekta hii kwa miaka ya nyuma. Kwa kiasi kikubwa nchi yetu imeanza kujitoa katika utegemezi wa malighafi, mashine, vifaa na hata wafanyakazi. Sasa nchi yetu imeanza kulinganisha Sekta za Viwanda na Kilimo kwa kuzifanya zitegemeane na imeweza kuimarisha masoko ya ndani na kuongeza usimamizi madhubuti wa mali za umma katika sekta hii. 

Wito wangu kwa watanzania, ipo haja ya kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa ubunifu wa juu ili kuchochea maendeleo ya Taifa kwa kuanza na maendeleo ya mtu mmoja mmoja. Kazi ya serikali ni kutoa mazingira wezeshi na nyenzo za maendeleo, tutumie nyenzo hizi kujikwamua kiuchumi kwa kutumia mbinu za kisasa katika kuendesha biashara zetu. Kila Mtanzania kwa nafasi aliyo nayo awajibike kutoa mchango wake kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na weledi.

MUNGU IBARIKI TANZANIA 
MUNGI IBARIKI AFRIKA

No comments