BASHE AHITIMISHA PROGRAMU YA KUFUNDISHA KWA KUJITOLEA NZEGA MJINI - "BASHE VOLUNTEERING PROGRAM 2018"
Nzega Mjini | Tabora,
Ni takribani miezi mitatu sasa toka mbunge wa Nzega Mjini Ndugu Hussein Bashe alipoanzisha programu maalumu ya walimu kufundisha kwa kujitolea iliyofahamika kama Bashe Volunteering Program.
Programu hii ilihusisha kukusanya walimu kutoka kwenye vyuo vikuu kumi na saba nchini; malengo ya program hii ni kuinua elimu na kuongeza kasi ya ufaulu miongoni mwa vijana ndani ya jimbo ili kuendeleza vita dhidi ya umasikini na kuandaa nguvu kazi kubwa hapo baadae itakayoshiriki katika uzalishajimali.
Jumla ya walimu 350 waliomba kushiriki lakini baada ya usaili ni walimu ndio walikuwa na sifa za kushiriki katika program hii.
Aidha walimu hao 67 waligawanywa kwenye shule Nane (8) za serikali ndani ya jimbo la Nzega Mjini lakini pia zoezi hili liliendana na uanzishwaji wa Makambi ya Walimu katika shule zilizo maeneo ya mbali ili kuwapa walimu muda wa kutosha kuweza kuwasaidia zaidi wanafunzi.
Ni kiu ya ndugu Hussein Bashe kuona Nzega inakua jamii iliyoendelea na kupungua kwa umasikini miongoni mwa wananchi hasa kwa kutumia elimu kama nyenzo ya msingi na ili kuhakikisha dhamira hii inakua katika vitendo mwaka huu pekee ndugu Hussein Bashe amelipia ada jumla ya wanafunzi 143 wa kidato cha Tano na Sita ndani ya jimbo la Nzega Mjini.
Bashe anasema ....."elimu kwetu ndio msingi wa maendeleo na ndio nyenzo ya kuondoa umasikini. Mataifa makubwa yote duniani yalipotaka kupiga hatua na kuendelea waliamua kuwekeza kwenye elimu"
Aidha, walimu hao walizawadiwa fedha ya akhsante kutokana na kazi kubwa waliyoifanya pamoja vyeti vilivyosainiwa na Waziri wa Elimu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bw.Philemon Magesa.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya wakiongozwa na Katibu Mwenezi CCM mkoa wa Tabora ndugu Majaliwa Bilali, Madiwani wa kata zote ndani ya Halmashauri ya Mji wa Nzega, Wakuu wa Shule zote za serikali na Watumishi kutoka Ofisi ya Afisa Elimu Nzega Mjini huku mgeni rasmi akiwa ni Makamu Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Tabora Mhe. Said Ntahondi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.
Makundi ya walimu, wadau wa elimu na wananchi wakiwa kwenye sherehe ya kuhitimisha programu
PICHA YA PAMOJA: Viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi, Serikali wakiwa kwenye Picha ya kumbukumbu na walimu waliokuwa kwenye programu "Bashe Volunteering Program"
No comments