Breaking News

WATENDAJI WA MITAA WATAKIWA KUSIMAMIA USAFI KWENYE MAENEO YAO

Na John Walter-Babati 

Watendaji wa Kata na mitaa wametakiwa kuhamasisha wananchi kufanya usafi katika mitaa na kata zao kila wiki ili kuweka maeneo yao katika hali ya usafi. 

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Babati mheshimiwa Mohamedi Kibiki akifungua kikao cha baraza la Madiwani kilichoketi jana na leo kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya mji wa Babati. 

Kibiki alisema katika mji wa Babati unaokuwa kwa kasi bado hali ya usafi wa Mazingira bado hairidhishi na kuamua kumuomba mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Fortunatus Fwema kuwasisitiza watendaji kusimamia zoezi hilo. 

Alisema anashangazwa kuona taka taka zikikaa muda mrefu bila kuzolewa licha ya kuwepo kwa gari la kazi hiyo akitolea mfano mtaa wa Osterbay alipopita na kukuta rundo la Taka taka likiwa bara barani siku mbili. 

“Sisi wananchi tuna majukumu mengi sana,wakati mwingine huwa tunasahau hata kutandika vitanda vyetu,kwa hiyo kuondoa karatasi ambayo ipo kwenye maeneo yako unaweza kusahau pia,lakini pakiwepo mtu wa kukumbusha basi tunaweza kuweka mazingira yetu tunayoishi katika hali ya Usafi”alisema Kibiki.

Sambamba na hayo aliwataka wananchi wanaoishi kwenye maeneo ambayo gari halifiki wajitahidi kuondoa taka taka zilizopo katika maeneo yao kwa kuteketeza kwa moto na wale wanaopitiwa na gari la taka waku kusanye zipitiwe na gari. 

Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo amesema hali ya upandaji miti katika mji wa Babati hairidhishi hivyo watendaji watiumize wajibu wao kwa kuhamasisha wananchi kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda na vivuli. 

Mji wa Babati ndio kitovu cha mkoa wa Manyara na kiunganishi cha mikoa mbalimbali ikiwemo makao makuu ya Tanzania jiji la Dodoma hivyo kama hautokuwa safi unaweza kuitangaza vibaya kwa wananchi na viongozi wanaopita katika mji huu.

No comments