Breaking News

TEKNOLOJIA MPYA YAANZA KUWAUMBUA WABUNGE WAKOROFI BUNGENI

Wabunge wasumbufu wanapokuwa ndani ya ukumbi wa Bunge, wamepatiwa mwarobaini baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusema anaweza kuwaona wabunge wote ukumbinu kupitia kwenye kifaa maalumu kilichofungwa kwenye meza yake.

Ndugai alisema hayo bungeni Dodoma jana alipokuwa akiendesha kikao cha 13 cha Bunge la 11.

Wakati Waziri Kivuli wa Fedha, Halima Mdee akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni juu ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2019/20, Ndugai alionekana kukemea wabunge waliokuwa wakipiga makofi kwa kutumia vitabu.

“Waheshimiwa wabunge siyo busara kutumia vitabu kupiga makofi, halafu mnatumia kitabu chenu (cha hotuba ya kambi ya upinzani) hiki.

“Siyo vizuri tumieni mikono, nawaona wote uipitia hiki kifaa hapa,” alisema Ndugai.

Pia katika kikao hicho cha asubuhi, kuna wakati wabunge walikuwa wakipiga kelele huku shughuli zikiendelea.

Spika Ndugai aliwakemea akitaja upande (wa upinzani au CCM) wenye kelele zaidi huku akisisitiza kuwa alikuwa anawaona wabunge hao kupitia kifaa hicho.

Kifaa hicho kipo kwenye kiti ambacho Spika ama mtu mwingine anayeongoza kikao cha Bunge huketi wakati Bunge likiendelea na kikao cha kawaida.

Kifaa hicho pia kipo eneo la makatibu wa Bunge ambako wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati, Mwenyekiti anayeongoza kikao hicho huketi eneo hilo.

Jana, Ndugai alitoa kauli hiyo wakati Bunge likiwa limekaa kusikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango, akiwasilisha Mpango wa Maendeleo ya Taifa na lilipokaa kama kamati ya mipango kusikiliza hotua ya Kamati ya Bajeti ya ile ya Kambi ya Upinzani.

Ndugai akiwa ameketi kama Spika na hata alipoketi kama mwenyekiti wa kamati ya mipango, alionekana akiwakemea wabunge kwa nyakati tofauti huku akisema alikuwa anawaona kupitia teknolojia hiyo.

Teknolojia hiyo, mbali na kusaidia kuona wabunge wasumbufu pia itasaidia kuona haraka Mbunge anayetaka kuuliza swali au kutoa hoja yoyote.

No comments